• HABARI MPYA

    Wednesday, April 16, 2014

    KATIKA HILI MKWASA AMETELEZA, BORA ANGEZUNGUMZIA TIMU YAKE ILIVYOPOTEZA POINTI SABA NDANI YA MECHI TATU

    NI miongoni mwa makocha bora na weledi Tanzania, Charles Boniface Mkwasa au Master ni mwalimu ambaye amepata mafunzo ya kitaaluma, tena ya kimataifa na amebobea.
    Ni kati ya walimu ambao nimewahi kufanya nao kazi na ninajua weledi na uhodari wao kazini- niseme ni miongoni mwa walimu ninaowaheshimu sana.
    Zaidi, nilimuona wakati anacheza katika nafasi ya kiungo alikuwa mchezaji mzuri kuanzia klabu yake Yanga SC hadi timu ya taifa, Taifa Stars ambako kote alipewa Unahodha.
     
    Kwa mara ya kwanza tangu namfahamu Mkwasa, mwishoni mwa wiki ndipo nilisikitishwa naye kwa matamshi yake aliyotoa wakati anazungumza na Waandishi wa Habari baada ya mchezo wa timu yake dhidi ya wenyeji JKT Oljoro mjini Arusha.
    Yanga SC ilitoka nyuma kwa bao 1-0 na kushinda 2-1, lakini ushindi huo haukuwasaidia kutunza taji la ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
    Hiyo ilitokana na waliokuwa wapinzani wao katika mbio za ubingwa, Azam FC kuwafunga 2-1 wenyeji Mbeya City na kufikisha pointi 59 ambazo haziwezi kufikiwa na timu nyingine yoyote- maana yake hao ndio mabingwa wapya wa nchi.
    Azam FC hadi kufikia kutambulishwa mabingwa wapya wa nchi Jumapili ya Aprili 13, 2014 hawajapoteza mechi hata moja- na hilo ndilo linalomuumiza Mkwasa akadai timu hiyo imetwaa taji hilo kimizengwe kwa sababu imeshinda mechi tano za ugenini.
    Haikuwa kauli inayofanana na kocha aliyepata mafunzo yake Ujerumani- na kwa ujumla haikuwa kauli inayofanana na mwalimu mweledi kama Mkwasa.
    Mkwasa amemdharau mwalimu mwenzake, Mcameroon Joseph Marius Omog ambaye mwaka jana aliipa Leopards ya Kongo ubingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika kabla hajatua Azam pamoja na wachezaji hata wamiliki wa Azam kwa kauli hiyo.
    Misimu mitatu iliyopita, Simba SC ilichukua ubingwa wa nchi bila kupoteza hata mechi moja na Yanga SC kwa bahati mbaya msimu uliopita walipoteza mechi moja tu, mbele ya Kagera Sugar. Je, nao walipata matokeo hayo kwa mizengwe? 
    Azam FC ilikuwa kwenye nafasi ya kuchukua ubingwa msimu uliopita, lakini ikafungwa mabao 2-0 na Mgambo JKT Uwanja wa Mkwakwani, Tanga hivyo kuwaacha Yanga wanyakue taji.
    Msimu huu, Yanga SC walikuwa katika nafasi ya kutwaa ubingwa, lakini wakapoteza pointi saba ndani ya mechi tatu, wakitoa sare ya bila kufungana na Mtibwa Sugar Uwanja wa Jamhuri Morogoro na sare ya 1-1 na Azam FC Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, tena wapinzani wote wakipoteza mchezaji mmoja mmoja kwa kadi nyekundu.
    Yanga SC iliyoshindwa kuzifunga Mtibwa na Azam pungufu, ikaenda kudondosha pointi zote tatu kwa kichapo cha mabao 2-1 kwa Mgambo JKT iliyopoteza mchezaji mmoja pia kwa kadi nyekundu.
    Katika sare ya 1-1 na Azam FC, Yanga walipoteza hadi penalti ambayo ingewapa bao la ushindi- baada ya Aishi Manula kuucheza mchomo wa Hamisi Kiiza.
    Haya ndiyo mambo ambayo Charles Boniface Mkwasa anatakiwa kuyazungumzia- ilikuwaje timu yake ikapoteza pointi saba ndani ya mechi tatu, tena ikicheza na timu zenye wachezaji pungufu na kupewa penalti pia.  
    Yanga SC iliifunga mabao 7-0 Ruvu Shooting. Ruvu Shooting iliifunga 1-0 Mtibwa Morogoro. Azam FC iliifunga 3-0 Ruvu Shooting Mlandizi. Lakini Yanga ilishindwa kuifunga Mtibwa pungufu Morogoro. 
    Yanga imekuwa ikipewa penalti karibu katika kila mechi za mzunguko wa pili na wapinzani pia wakipunguziwa wachezaji kwa kadi nyekundu- je hiyo nayo ni mizengwe?
    Hapana. Soka inaongozwa na sheria 17, kuunawa mpira ndani ya mita 18 au kuchezea rafu kwenye eneo hilo ni penalti. 
    Unapocheza rafu, kutoa lugha chafu au kuonyesha utovu wa nidhamu wa aina yoyote, refa ana wajibu wa kutoa adhabu- hivyo kama wapinzani wa Yanga SC walistahili adhabu hizo hakuna mizengwe.
    Erasto Nyoni wa Azam alistahili kadi nyekundu katika mechi dhidi ya Yanga, baada ya akiwa tayari ana kadi ya njano akamtukana refa Hashim Abdallah. Azam ilistahili kucheza pungufu na pongezi kwao kwa kupata sare ya 1-1 tena wakinusurika na tuta la Kiiza.
    Hakuna mizengwe. Mkwasa anaweza kuujua uwezo wake, lakini si uwezo wa mtu mwingine na zaidi alitakiwa kufanya kile kitu ambacho wenye soka yao wanaita Fair Play, kwa kuwaambia ‘Hongereni Azam’.

    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KATIKA HILI MKWASA AMETELEZA, BORA ANGEZUNGUMZIA TIMU YAKE ILIVYOPOTEZA POINTI SABA NDANI YA MECHI TATU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top