• HABARI MPYA

    Thursday, September 25, 2014

    KWIZERA, KIONGERA WAPATIWA VIBALI VYA KUPIGA KAZI SIMBA SC, CHA OKWI CHADUNDA…SABABU HAIJULIKANI

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    IDARA ya Uhamiaji Tanzania imetoa vibali vya kufanyia kazi kwa wachezaji wawili wa Simba SC, Mrundi Pierre Kwizera na Mkenya Paul Kiongera pamoja na kocha wao, Patrick Phiri, lakini haijatoa kibali cha mshambuliaji Mganda Emmanuel Okwi.
    Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe ameiambia BIN ZUBEIRY jioni hii kwamba wamefanikiwa kupata vibali vya wachezaji hao na kocha Phiri, lakini pamoja na kupeleka pia maombi kwa ajili ya kibali cha Okwi, hakijatoka.
    “Bado hatujajua sababu za kutotoka kwa kibali cha Okwi, lakini tunaendelea kufuatilia ili tujue, kwa sababu huyu ni mchezaji wetu halali, ambaye tulikamilisha taratibu za kumsajili baada ya mkataba wake na klabu yake ya awali, Yanga SC kuvunjika,”amesema Poppe.
    Pierre Kwizera atapiga kazi kama kawaida Simba SC baada ya kupatiwa kibali

    Mapema jana, Idara ya Uhamiaji iliwazuia wanne hao kufanya kazi Simba SC hadi hapo watakapopatiwa vibali- lakini sasa wanaweza kuendelea na kazi, kasoro Okwi ambaye kibali chake kimekwama.
    Simba SC inashuka dimbani Jumamosi hii kumenyana na Polisi Morogoro katika mfululizo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na maana yake iko hatarini kumkosa Okwi.
    Okwi anaweza kukosekana katika wakati ambao Simba SC inamkosa mshambuliaji mwingine, Kiongera ambaye ni majeruhi anayetakiwa kuwa nje kwa wiki sita.
    Simba SC pia itawakosa kipa Ivo Mapunda, beki Issa Rashid ‘Baba Ubaya’ na winga Haroun Chanongo ambao wote ni majeruhi, lakini habari njema tu ni kwamba kiungo ‘mchapakazi’ Jonas Mkude yuko tayari kuanza kazi Jumamosi.
    Mapunda ni majeruhi wa muda mrefu kama Kiongera, ambaye anatakiwa kuwa nje kwa wiki nane, wakati Issa na Chanongo wiki ijayo wanaweza kurudi kazini.
    Haijulikani ‘zengwe’ la Okwi litachukua muda gani kumalizika kabla ya mchezaji huyo kurejea uwanjani.
    Simba SC ilianza Ligi Kuu kwa sare ya 2-2 na Coastal Union ya Tanga Uwanja wa Taifa, Jumapili iliyopita licha ya kuongoza kwa 2-0 hadi mapumziko- maana yake itahitaji ushindi Jumamosi ili kujiweka mguu sawa katika mbio za kuwania ubingwa. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KWIZERA, KIONGERA WAPATIWA VIBALI VYA KUPIGA KAZI SIMBA SC, CHA OKWI CHADUNDA…SABABU HAIJULIKANI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top