• HABARI MPYA

    Wednesday, September 10, 2014

    SIMBA SC NA YANGA WAPEWA JEZI ‘SARE SARE MAUA’ NA VODACOM KWA AJILI YA LIGI KUU

    Na Renatus Mahima, DAR ES SALAAM
    WADHAMINI wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Vodacom wametoa kezi zinazofanana kabisa kwa mahasimu wa jadi nchini, Simba na Yanga SC- tofauti ni moja tu, rangi.
    Katika hafla ya kukabidhi vifaa kwa timu za Ligi Kuu msimu mpya leo, Vodacom wamekabidhi jezi za rangi ya kijani na njano kwa Yanga na nyekundu na nyeupe kwa Simba, lakini muundo ni mmoja kila kitu.
    Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) liliwakilishwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ ambaye alihakikisha timu zote 14 za Ligi Kuu zinapatiwa vifaa hivyo.
    Sare sare maua; Kulia ni jezi ya Simba SC na kushoto jezi ya Yanga ambazo wamekabidhiwa leo na wadhamini Vodacom, kwa ajili ya Ligi Kuu

    Timu zote 14 zilituma wawakilishi wao katika hafla hiyo iliyofanyika makao makuu ya Vodacom, Mlimani City, Dar es Salaam.  
    Ligi Kuu inatarajiwa kuanza Septemba 20, mwaka huu, mabingwa watetezi, Azam FC wakifungua dimba na Polisi Morogoro Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
    Yanga SC waliomaliza nafasi ya pili wataanza na Mtibwa Sugar Uwanja wa Jamhuri, Morogoro siku hiyo, wakati washindi wa tatu, Mbeya City wataanza na JKT Ruvu ya Pwani, Uwanja wa Sokoine, Mbeya Septemba 20.
    Mwakilishi wa Azam FC, Philipo Alando kulia akipokea jezi kutoka kwa wadhamini leo

    Mechi nyingine za ufunguzi za Ligi Kuu zitakuwa kati ya Stand United watakaoikaribisha Ndanda ya Mtwara Uwanja wa Kambarage, Shinyanga, Mgambo JKT wataikaribisha Kagera Sugar Uwanja wa Mkwakwani, Tanga na Ruvu Shooting watakuwa wenyeji wa Prisons Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani.
    Mabingwa wa zamani wa ligi hiyo, Simba SC wataanza kampeni ya kutwaa tena taji hilo Septemba 21 dhidi ya Coastal Union Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Ligi hiyo itatanguliwa na mchezo wa Ngao ya Jamii utakaochezwa Jumapili wiki hii, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kati ya Azam FC na Yanga SC.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA SC NA YANGA WAPEWA JEZI ‘SARE SARE MAUA’ NA VODACOM KWA AJILI YA LIGI KUU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top