• HABARI MPYA

    Friday, September 12, 2014

    SIMBA SC WACHAPWA 1-0 NA OKWI NA KIONGERA WAO, URA NOMA HAWANA KUCHOKA

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    SIMBA SC imepoteza mechi ya kwanza chini ya kocha Mzambia, Patrick Phiri baada ya jioni ya leo kufungwa bao 1-0 na URA ya Uganda katika mchezo wa kirafiki Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Bao hilo pekee la timu hiyo ya Mamlaka ya Mapato Uganda lilifungwa na Frank Kalanda dakika ya 42, akimalizia krosi ya Elkanda Nkungwa aliyefanikiwa kumtoka Mohammed Hussein ‘Tshabalala’. 
    Pamoja na kufungwa, Simba SC ilicheza vizuri na jioni ya leo bahati haikuwa ya kwao, kwani walipoteza nafasi zisizopungua tano za kufunga mabao.
    Mshambuliaji wa Simba SC, Emmanuel Okwi kushoto akiwatoka mabeki wa URA ya Uganda jioni ya leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. URA ilishinda 1-0.

    URA pamoja na kuwasili Saa 6:00 usiku wa jana, lakini haikuonyesha uchovu badala yake ‘iliipelekesha’ Simba SC na kama si jitihada za kipa Ivo Mapunda kuokoa michomo mingi ya hatari, wangeweza kupata mabao zaidi.
    Baada ya mchezo wa leo, SImba SC inaelekea Mtwara mapema asubuhi ya kesho kuungana na wachezaji wengine waliotangulia wakiongozwa na Amisi Tambwe kwa ajili ya mechi na Ndanda, ya kirafiki pia.
    Mchezo na Ndanda ndiyo utakuwa wa mwisho kwa Simba wa kujipima nguvu kabla ya kuanza kwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara wiki ijayo, Wekundu hao wa Msimbazi wakifungua dimba na Coastal Union ya Tanga Septemba 22, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.   
    Awali, Simba SC chini ya Phiri aliyerithi mikoba ya Mcroatia Zdravko Logarusic mwezi uliopita, ilishinda 2-1 dhidi ya Kilimani FC, 2-0 dhidi ya Mafunzo na 5-0 dhidi ya KMKM zote Uwanja wa Aamaa, Zanzibar na 3-0 dhidi ya Gor Mahia ya Kenya, Uwanja wa Taifa.
    Simba SC; Ivo Mapunda, Miraj Adam, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Hassan Isihaka, Joseph Owino, Pierre Kwizera, Ramashani Singano ‘Messi’, Amri Kiemba/Paul kiongera dk49, Emmanuel Okwi, Shaaban Kisiga na Haroun Chanongo/Uhuru Suleiman dk62.
    URA; Bwete Brian, Massa Simeon, Munaabu Alan, Samuel Ssenkoom/Ronald Sekubomba dk64, Jonathan Mugabi, Oscar Agaba, Feni Ali, James Kasibante/Ngama Emmanuel dk57, Said Kyeyune, Elkanda Nkugwa/Augustino Nsumba dk64na Frank Kahanda. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA SC WACHAPWA 1-0 NA OKWI NA KIONGERA WAO, URA NOMA HAWANA KUCHOKA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top