• HABARI MPYA

    Saturday, October 18, 2014

    KAMA CASILLAS, KWA NINI SIYO MANYIKA JR.

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    UPO uwezekano mkubwa, kipa chipukizi, Peter Manyika akasimama langoni leo kuidakia timu yake, Simba SC dhidi ya mahasimu Yanga SC katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
    Simba SC imemsajili msimu huu kipa huyo wa timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20 katika kikosi chake cha cha pili, na ikaamua kumpeleka kikosi cha kwanza kumkomaza.
    Ndani ya Simba SC, gumzo kubwa kuhusu mtoto huyo wa kipa wa zamani wa kimataifa wa Tanzania ni kwamba, ndiye kipa namba moja wa baadaye wa klabu hiyo.
    Lakini baada ya kutokea dharula ya makipa wake wote wa timu ya kwanza kuumia, Ivo Mapunda na Hussein Sharrif ‘Casillas’ matumizi ya Manyika Jr. yamekuja mapema kuliko ilivyotarajiwa.
    Mapunda aliumia kidole wiki ya mwisho ya Septemba na akatakiwa kuwa nje kwa wiki nane, lakini kufuatia Casillas kuumia ugoko kambini Afrika Kusini, Ivo alipandishwa ndege kwenda Johannesburg Jumatatu wiki hii.
    Baada ya kufika Afrika Kusini, Ivo kwanza alifanyiwa vipimo na baadaye akaongezewa tiba ili awe fiti tayari kudaka Jumamosi ya leo.
    Peter Manyika anahitaji kuaminiwa na kupewa muda kabla ya kuwa kipa tegemeo Simba SC

    Lakini wana Simba SC hawaamini kama Ivo atakuwa tayari kudaka leo na wakati huo huo hawaamini kama ‘dogo’ Manyika anaweza kuhimili vishindo vya pambabo la watani.
    Ukweli ni kwamba, kumpanga Ivo leo ni kulazimisha kwa sababu ya uzoefu wake, lakini maumivu ya kidole gumba yanaweza kumfanya adake kwa mkono mmoja, jambo ambalo ni hatari zaidi.
    Tayari Manyika mdogo amekwishadaka mechi tatu za kirafiki katika kambi ya Simba SC nchini Afrika Kusini, ya kwanza akiingia dakika ya 43 kumpokea Casillas katika sare ya 0-0 na Orlando Pirates ya pili timu hiyo ikifungwa 4-2 na Bidvest Wits na ya tatu Wekundu wa Msimbazi wakifungwa 2-0 na Jomo Cosmos.
    Inaaminika soka ya Afrika Kusini ipo juu maradufu kuliko ya Tanzania- na Simba ilicheza ugenini, tena kwa tahadhari bila kutumia nguvu nyingi kuhofia wachezaji wake kuumia kabla ya mechi na Yanga.
    Hivyo basi, kufungwa haimaanishi moja kwa moja ni timu dhaifu. Lakini wakati mwingine timu inaweza kufungwa si kwa sababu ya udhaifu wa kipa, bali udhaifu wa timu au makosa ya mabeki.
    Manyika mdogo hakuwepo langoni wakati Simba SC inafungwa 3-0 na ZESCO United Agosti mwaka huu, bali kaka zake Ivo na Casillas walipokezana.
    Mwezi uliopita niliandika makala, ikielezea namna ambavyo ni rahisi Simba SC kuua kipaji cha Manyika mdogo- sababu ni pamoja na hii, ni vigumu kuaminiwa na kupewa nafasi hata itakapobidi.
    Sasa imetokea dharula, inayolazimisha dogo huyo aanze mapema kazi Msimbazi, watu wanakuna kichwa kumpanga kiasi cha kutaka kulazimisha Ivo adake japokuwa ni majeruhi.
    Kama Simba SC inaamini Manyika ndiye kipa wake wa baadaye wa kwanza- ianze kumuandaa sasa kwa kumuamini kumpa mechi, tena na isiwe tayari kumnyima amani hata ikitokea akafanya vibaya kwenye mchezo huo.
    Lakini matumaini makubwa ni Manyika kufanya vizuri, kwa sababu ni kipa mzuri, ambaye amedhihirisha uwezo wake tangu anadakia timu ya vijana chini ya umri wa miaka 17, tena aliyedhamira kufuata nyayo za baba yake, aliyewahi kuitwa Tanzania One enzi zake.
    Iker Casillas, kipa wa Real Madrid kwa sasa uwezo wake unaelekea ukingoni baada ya kuwika tangu muongo uliopota- lakini ukirejea historia yake unagundua siri ya mafanikio yake ni kuaminiwa na kupewa nafasi tangu angali kinda. 
    Casillas ametokea kwenye mfumo wa soka ya vijana wa Real Madrid, unaofahamika kama La Fabrica msimu wa 1990–1991 na kufika Novemba 27, 1997 akiwa na umri wa miaka 16 aliitwa kwa mara ya kwanza kwenye kikosi cha kwanza cha Real kwa ajili ya mechi na Rosenborg kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya.
    Hata hivyo, hakupewa nafasi hadi msimu wa 1998–1999  alipotokea benchi kuchukua nafasi ya Bodo Illgner na msimu uliofuata akafanikiwa kumpokonya namba Illgner na kuwa kipa wa kwanza.
    Mwaka 2000, akaweka rekodi ya kuwa kipa mdogo zaidi kudaka katika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya wakati Real Madrid ilipoifunga Valencia mabao 3–0, siku nne tangu atimize miaka 19.
    Casillas wa Real alijiamini na akafanya kazi kwa sababu aliaminiwa kwanza- vivyo hivyo kwa Simba SC, wakimuamini Manyika mdogo, naye anaweza kujiamini na akafanya kitu ambacho wengi hawatarajii kwa sasa. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KAMA CASILLAS, KWA NINI SIYO MANYIKA JR. Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top