• HABARI MPYA

    Wednesday, December 17, 2014

    HUU NDIO UKWELI WA ASILIMIA 90 KUHUSU KIFO CHA AISHA MADINDA

    HUU NDIO UKWELI WA ASILIMIA 90 KUHUSU KIFO CHA AISHA MADINDA …aliondoka nyumbani jana na hakurudi tena, madawa ya kulevya yahusishwa

    Kifo cha mnenguaji Mwainaisha Mohamed Mbegu “Aisha Madinda” aliyefariki leo, kimeleta utata kwa namna kilivyotokea.
    Saluti5 inakuletea kwa muhtasari wa namna kifo cha Aisha Madinda kilivyotokea, hii ikiwa ni kwa mujibu wa ndugu na marafiki wa marehemu waliokusanyika hospitali ya Mwananyamala hadi muda huu.
    Mtoto wa kwanza wa marehemu, Feisal ameiambia Saluti5 mama yake ambaye alikuwa haumwi chochote, aliondoka nyumbani juzi na hakurejea tena.
    Feisal anasema jana aliongea na mama yake kwa njia ya simu kwa zaidi ya mara tatu na akamwambia yuko Mabibo kwa rafiki yake aitwaye Samira.
    Lakini Samira anasema Aisha Madinda hakuwa kwake hiyo jana lakini alimkuta barazani kwake (Mabibo) asubuhi ya leo akiwa hajitambui.
    Samira anasema alijitahidi kumtingisha lakini Aisha Madinda alikuwa kimya na hivyo akaamua kuchukua bajaji na kumkimbiza hospitali ya Mwananyala.
    Rafiki huyo wa Aisha Madinda anasema alifika Mwananyamala Hospitali majira ya saa 2 asubuhi na daktari aliyempokea akamwambia tayari mgonjwa wake alishafariki dunia.
    Samira anasema, yeye kama alivyo Aisha Madinda, ni muathirika wa madawa ya kulevya ambapo anaitaja hospital ya Mwananyamala ndio kliniki yao ya kupata tiba saidizi (MAT) ya madawa ya kulevya na ndio sababu hakumpelekea hospitali nyingine yoyote zaidi ya Mwananyamala.
    Kinachoshukiwa: Marafiki wa Aisha Madinda ambao nao ni waathirika wa madawa ya kulevya, wanadai Aisha Madinda alirudia utumiaji wa madawa ya kulevya na hivyo wana mashaka kuwa alitumia kiasi kikubwa kuliko inavyohitajika na pengine ndio sababu ya kifo chake.
    Ndugu wanasemaje? Ndugu wa marehemu akiwepo dada yake ambaye ndio wa kwanza kuzaliwa, Amida Mohamed Mbegu, ameiambia Saluti5 kuwa hadi sasa wameadhimia kukubali kazi ya Mungu na hawatarajii kuufanyia upasuaji mwili wa marehemu ili kujua chanzo cha kifo chake.
    Maisha yake katika siku za hivi karibuni:
    Ndugu wa marehemu wanasema katika siku za hivi karibu, Aisha alikuwa akiondoka nyumbani kwao Kigamboni asubuhi na kusema anaelekea kwenye mazoezi ya Twanga Pepeta kwaajili ya onyesho la miaka 16 ya Luizer Mbutu.
    Lakini kiongozi wa madansa wa Twanga, Danger Boy ameiambia Saluti5 kuwa Aisha Madinda hajawahi kuonekana kwenye mazoezi ya bendi yao.
    Kiongozi wa Twanga Pepeta, Luzier Mbutu naye amekiri kuwa licha ya Aisha Madinda kumwahidi mara kadhaa kwa njia ya simu kuwa atashiriki mazoezi, lakini hakuwahi kutokea hata mara moja.
    Mazishi yake: Mwili wa marehemu umehifadhiwa chumba cha maiti cha Hospitali ya Mwananyamala na mazishi yatafanyika Kigamboni kesho saa 10.
     Hamida Mbegu dada wa Aisha Madinda
     Feisal mtoto wa kwanza wa Aisha Madinda
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: HUU NDIO UKWELI WA ASILIMIA 90 KUHUSU KIFO CHA AISHA MADINDA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top