• HABARI MPYA

    Tuesday, December 16, 2014

    MAXIMO ATUPIWA VIRAGO YANGA SC, ‘BABU’ PLUIJM AWASILI DAR KUPIGA KAZI NA MKWASA

    Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
    YANGA SC imevunja benchi lake zima la Ufundi, ikiwaondoka makocha Wabrazil, Marcio Maximo na Msaidizi wake, Leonardo Leiva na kuwarejesha Mholanzi, Hans van der Pluijm na mzalendo, Charles Boniface Mkwasa.
    Maximo anaondolewa baada ya kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa mahasimu Simba SC Jumamosi katika mchezo wa Nani Mtani Jembe, wakati Pluijm anawasili usiku huu na kesho atasaini Mkataba na kuanza kazi. Mkwasa tayari alisaini Mkataba wiki kadhaa zilizopita na ameridhika kufanya kazi chini ya Pluijm tena.
    Maximo na Leonardo walitua Yanga SC Julai mwaka huu kurithi mikoba ya Pluijm na Mkwasa ambao walipata kazi Uarabuni. Hata hivyo baada ya muda usiozidi mwezi mmoja, Pluijm na Mkwasa waliacha kazi Uarabuni, wakidai kukerwa na kuingiliwa na viongozi wa klabu yao katika masuala ya kiufundi.
    Hans van der Pluijm anawasili usiku huu kumrithi Maximo Yanga SC

    Pluijm alirudi Ghana wakati Mkwasa alirejea nyumbani Tanzania kabla ya kuajiriwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kama Mkufunzi Mkuu.
    Hadi anaondoka Yanga SC, Maximo ameiongoza timu hiyo katika mechi 14, kati ya hizo akishinda 10, sare moja na kufungwa tatu dhidi ya Kagera Sugar 1-0, Mtibwa Sugar 2-0 sawa na Simba SC katika Mtani Jembe.  
    Pluijm aliiongoza Yanga SC katika mechi 19, akishinda 11, sare sita na kufungwa mbili dhidi ya Al Ahly 1-0 Cairo na Mgambo JKT 2-1 Tanga.
    Yanga SC ilikuwa tayari kuendelea na Maximo iwapo angekubali kufanya kazi na Mkwasa, lakini baada ya kukataa, klabu imeoana bora kuachana naye.
    Maximo alikuwa anafanya kazi kwa mara ya pili Tanzania, baada ya awali kuwa kocha wa timu ya soka ya taia, Taifa Stars kuanzia mwaka 2006 hadi 2010.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MAXIMO ATUPIWA VIRAGO YANGA SC, ‘BABU’ PLUIJM AWASILI DAR KUPIGA KAZI NA MKWASA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top